SOMO: VITU VITAKAVYO KUSAIDIA UISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI
MWL. KELVIN KITASO ....... 0713804078
1. Kuishi kwa malengo.
Ukiwa na malengo katika maisha yako ni lazima utumiaji wa muda utakuwa ni tofauti na wengine wanavoweza kutumia. Lazima uwe na malengo kwa kufahamu unataka nini katika maisha. Watu wote wanaofanikiwa huwa ni watu ambao wanamalengo, yaani wanafahamu wanahitaji nini? Ukiwa haujui unachokihitaji katika maisha kila kitu utakachokifanya katika maisha yako bado utakiona kipo sawa.
Malengo ndiyo yatakufanya usitulie, ndiyo yatakayoongoza maamuzi yako na ndiyo yatakayokuwa kiongozi katika kutumia muda wako.
2. Orodhesha mambo ya kufanya mara kwa mara kabla haujaanza kufanya.
Ni vibaya kuamka asubuhi hujui unafanya nini, au unaenda wapi au unapaswa kukamilisha nini kwa siku hiyo. Ukiwa unaishi katika mfumo wa maisha kama hayo chochote kwako kikitokea utaona ni sawa, ukishawishiwa kwenda popote bado utaona ni sawa na utakubali kwenda.
Ni vyema zaidi kila siku ikawa na ratiba maalumu ya nini unapaswa kufanya kwa siku hiyo na wapi unapaswa kuelekea katika siku hiyo. Paulo alipokuwa anawaandikia waraka Wathesalonike aliwaonya wawe watu wanaoenenda kwa utaratibu, kuenenda kwa utaratibu ni kuwa watu ambao wanajua nini wanapaswa kukifanya na kwa muda gani na kisha kukifanya. Usipokuwa na maarifa ya kufahamu nini unapaswa kufanya kwa siku hiyo si rahisi ukafanikiwa.
Kila siku inapoanza lazima uwe unajua kuwa kwa leo napaswa kukamilisha jambo Fulani, na hakikisha kuwa linakamilika. Usikubali kuimaliza siku yako bila kukamilisha lile ambalo ulipaswa kulikamilisha.
Rafiki yangu Christina huwa anapenda kunisisitiza kuwa hatuendi kulala kwa kuwa usiku umeingia ila tunalala kwa kuwa tuliyopaswa kuyakamilisha kwa siku ya leo tumeyakamilisha kwa ukamilifu, na kisha kumshukuru Mungu atupaye nguvu ya kukamilisha. Na siku ikianza tu bila kumuomba nguvu za kuikamilisha mipango huwa ni siku nzito sana, siku moja alinipigia simu akihudhunika kuwa siku yake imekuwa mbaya sana, nikamuuliza kwa nini? Akanieleza kuwa aliondoka nyumbani bila ya kumuomba Mungu amtangulie ndiyo maana ameteseka sana.
Unapolala mshukuru Mungu kwa kukupa nguvu ya kufanikisha yale uliyokuwa nayo kwa hiyo siku, na unapoamka muombe Mungu akupe nguvu tena ya kutekeleza yale uliyonayo kwa siku ya leo.
Nimejifunza kwa mtumishi wa Mungu Nabii T.B Joshua anayesema kabla ya mambo yote mkabidhi Mungu mambo yako kwa kumwambia, Oh! Lord Jesus, take more of me, and give me more of you” yaani, “Bwana Yesu, chukua yaliyo yangu na unipe yaliyo yako”
Watu wanaofanikiwa ni watu ambao wanaenenda kwa utaratibu na wanaratiba kila siku za kufanya na ndiyo maana ukihitaji kuonana na watu waliofanikiwa si rahisi ukakurupuka tu na ukafika ofisini kwao na ukawakuta, kwa kuwa kila dakika yao imepangiliwa, ila watu ambao hawajui kwenda kwa utaratibu ni rahisi sana kupatikana kila wakati kwa kuwa wanamuda na dakika za kutosha na hata wakiupoteza hawapungukiwi na kitu.
3. Ishi maisha ya vipaumbele.
Kuwa na vipaumbele katika vile vingi ulivyonavyo kutakusaidia sana kutumia muda wako vizuri na kukuzalia matunda mazuri. Uwe na concentration katika vipaumbele vyako vya hiyo siku. Kama umesema kuwa naanza kusoma kitabu Fulani, hakikisha unasoma mpaka unakimaliza ndipo upate nguvu ya kuendelea na mengine.
Watu wengi wanafanya vitu lakini hawana concentration katika yale wanayoyafanya na ndio maana huwa hawamalizi, unakuta mtu anaanza kitu Fulani hakimalizi na anaishia katikati.
4. Jiwekee muda wa kukamilisha (deadline).
Ili uweze kuwa mtumiaji mzuri wa muda usianze tu kitu halafu ukawa unafanya fanya tu. Jiwekee muda wa kumaliza hiko kitu unachokifanya, deadline itakuwa ni nguvu inayokusukuma kufanya kile ulichonacho.
Wakati Mungu anafanya uumbaji alijiwekea muda kuwa mpaka kufikia siku 7 ni lazima uumbaji uwe umekamilika na ndivyo alivyofanya, kila siku akaipa majukumu yake ili tu kuhakikisha anakamilisha kile alichoadhimia kukifanya, ila pia aliweka vipaumbele katika vile alivyofanya, alikusudia kumuumba mwanadamu ila hakumuumba siku ya kwanza, utagundua hakumuumba siku ya kwanza kwa kuwa hakikuwa kipaumbele chake cha kwanza katika uumbaji wake lakini pia kama angemuumba siku ya kwanza angekuja kufanya nini kama angekuta kila kitu bado hakijaumbwa na udongo wa kumfinyangia angeutoa wapi?. Mungu akaona huyu awe wa mwisho ili akute kila kitu.
Tengeneza udongo kwanza kabla hujaanza kuumba
Utagundua kipaumbele cha Mungu ilikuwa ni kuanza na mengine kwanza ikiwemo udongo ili kazi ya kuumba isije kuwa ngumu. Na masaa 24 ya mwisho tayari alikuwa na udongo hivyo akayatumia vizuri sana masaa hayo kwa ustadi mkubwa kumtengeneza mwanadamu.
Unapoanza ni vyema ukaanza na kutengeneza udongo kwanza utakaokusaidia kutengeneza kile unachokitaka, usianze kuumba mtu wako kabla hujawa na udongo, na ukikosea hapo kazi ya masaa 24 utaifanya kwa miaka 24 na bado haitakamilika.
Hata wewe unavyofanya mipango ya maisha yako ni lazima uweke orodha ya vitu muhimu, kisha ujiwekee muda wa kuvikamilisha, kisha uchague vipi vya kuanza navyo na uanze kuvifanyia kazi. Hata kama ni malengo yako usifanye kila kitu kwa huo wakati, fanya vyenye kipaumbele tu.
5. Anza kufanya sasa.
Usiseme kuwa nitafanya, anza kufanya sasa. Wengi wanamipango mizuri na haitimii kwa kuwa ni wavivu wa kutendea kazi na mara nyingi husema nitafanya. Katika kuukomboa wakati, hakikisha unaanza sasa na uanzie pale ulipo.
Tafakari kama Mungu angesema “tutaumba” nafikiri mpaka sasa angekuwa anaahirisha ikimjia ratiba nyingine angekuwa anaahirisha tu, ila yeye alisema “natumfanye” maanaake tuanze kufanya sasa. Hauna muda wa kupoteza kuwa nasubiri nipate hela ndipo nianze.
Anza hapo hapo ulipo tengeneza jitihada za kutosha ndipo mafanikio ya kweli yanatokea kwa namna hiyo. Kumbuka kuwa huna muda wa kusubiri kuanza hilo unalotaka kulianza. Muda mzuri wa kuanza ni sasa.
Watu wanaofanikiwa ni watu wanaothubutu kuanza kufanya bila kusubiri chochote ila watu wengi wasio fanikiwa hawafanikiwi kwa sababu huwa hawaanzi kufanya, wanapenda kusubiri subiri. Utawasikia wanasema nikipata milioni 1 nitaanza biashara, ila wanaofanikiwa wakipata hata 10,000/= huwa wanaanza bila kusubiri.
6. Achana na kila kinachokupotezea muda.
Inaweza ikawa ni watu unaoshirikiana, mitandao, video unazoangalia. Kuwa makini kuachana navyo vyote maana vinaweza kukuharibia malengo uliyonayo.
Watu wengi wanaweza kuwa ni wapoteza muda tu, na hakuna vitu vya msingi mnavyoweza kuvifanya kuwa na future iliyonjema. Watu kama hao achana nao. Unaweza ona mtu anapiga simu muda wa kazi na anakuambia nimekumiss nilikuwa nataka kukusalimia. Ni nzuri inahimarisha ushirikiano ila haina umuhimu kwa kuwa ni wakati wa kutekeleza majukumu mengine. Mtu akikupigia simu wakati wa kutekeleza majukumu yako si lazima kuipokea simu yake kwa kuwa inaweza kuambatana na taarifa ambazo zinaweza kukutoa katika majukumu unayoyafanya.
Kama kuchati kunakupotezea muda achana nako ili utimize mambo ya msingi. Ukweli ni kwamba kuchati hakuna hatima nzuri ya maisha yako, kuwa makini kila wakati na namna unavyofanya, kuna watu wapo makundi ya kuchati mengi sana na mengi yao hayana hata faida kwao ila wamo tu, tafsiri yake hawa ni aina ya watu ambao hawajui wapi wanaelekea. Watu wanaojielewa huwezi kuwakuta wanachati chati tu bila mpangilio au wapo kwenye makundi mengi yasiyo na maana na hata ukiwakuta kwenye makundi ujue kuna mambo ya msingi wanafanya au wanayatumia kwa faida ya kufikia malengo yao.
Ili kubadilika unahitaji kubadilika.
7. Fanya tathmini juu ya malengo unayojiwekea
Katika malengo uliyojiwekea katika siku hiyo kabla hujalala jipe muda wa kujitathimini ni mangapi umeyatimiza na mangapi haujayatimiza, nay ale ambayo hujayatimiza ni nini kimekusababisha usitimize, ili kesho uhakikishe unakuwa makini kutorudia kosa lile lile.
Mfano mzuri ni Mungu mwenyewe kila siku alipokuwa akimaliza majukumu yake alifanya tathmini ya kazi yake na akahitimisha kwa kusema kila kitu kilienda vyema. Hakuanza shughuli za siku ya pili kabla ya kufanya tathmini ya siku ya inayoisha.
WAWEZA AGIZA NAKALA ZA KITABU CHA MAMBO 20 YATAKAYOKUFANYA UFURAHIE MAISHA YAKO KUPITIA NAMBA 0713 804 078.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni