Jumatatu, Agosti 15, 2016

MALEZI YA MTOTO (SEHEMU YA PILI)

NAFASI YA MZAZI

MWL. KELVIN KITASO

CHUKUA MUDA WA KUTOSHA KUSOMA JAPO NI REFU
Wazazi wengi wamekuwa na imani kuwa kazi yao kubwa ni kuzaa, kwa kutimiza lile kusudi la Mungu la kuzaa na kuongezeka na kusahau kuwa baada ya kuzaa na kuongezeka kuna kazi ya ziada ambayo inapaswa kufanywa na wazazi kama watu waliopewa dhamana ya kumiliki uzao wao.  Mzazi yeyote ili kuwa mzazi bora ni lazima aige ni kwa namna gani Mungu analea watoto wake kwa kuwa Mungu ni Baba, ni vyema kwa kila mzazi kuangalia ni kwa namna gani Mungu kama Baba anafanya mpaka watoto wake huwa na tabia njema ambayo haifanani kabisa na ya watoto wengine.
Kitabu cha Isaya 48:17 “……..Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.” Kitabu hiki cha Isaya Mungu anajitambulisha kwa watoto wake ni nafasi gani aliyo nayo kama mwalimu na kama kiongozi mbele za watoto wake. Nafasi hizi ndizo alizo nazo mzazi mbele ya wanae.
Zipo nafasi ambazo anazo mzazi katika malezi ya mtoto nazo ni kama:
1.    KIONGOZI
Mzazi ni kiongozi katika familia na chini yake anao wafuasi wake ambao uitwa watoto na viongozi hawa uwa ni katika ngazi kuu mbili, yaani kiongozi mkuu (mwenyekiti) ambaye mara zote huwa ni baba na msaidizi wake ambaye ni mama (katibu). Viongozi hawa ndio wakuu ambao huanzisha taasisi yao na katika taasisi yao hupatikana watoto, hakuna taasisi isiyo na maono, hivyo viongozi hawa uhusika kutoa mwelekeo kwa wafuasi wao ni kwa namna gani taasisi yao inapaswa kuwa na washirika wa hiyo taasisi wanapaswa kuweje. Kuna nyakati kiongozi huwa na demokrasia lakini kuna wakati ulazimika kufanya maamuzi ya kidikteta kulingana na aina ya wakati uliopo. Ndivyo ilivyo kwa wazazi kwa kuwa kuna wakati watakuwa na hali ya demokrasia na kuna wakati watakuwa na hali ya udikteta ili kuhakikisha mambo yanaenda vyema katika familia. Mzazi akifaulu kuelewa kiongozi hupaswa kuwaje ni lazima atakuwa mtu wa tofauti kuwasaidia watoto wake kufanya vizuri.
Kiongozi ni mtu anayejua njia, anatembea katika njia na kuonyesha njia kwa wafuasi wake. Na ndiyo nafasi kuu waliyonayo wazazi katika familia kama kiongozi.

Kujua njia
Kujua njia ni sehemu ndogo tu, ila ni ya msingi sana kwa mzazi yeyote yule kuijua njia ipasayo kupitiwa, na ni muhimu kufahamu kuwa kama kiongozi hajui njia ni rahisi sana kuwapoteza watu wake na kuwafanya wakapotea njia. Yesu Kristo ni njia na kweli na uzima, Yesu ambaye ni njia uitwa neno. Njia ni neno la Mungu. Maandiko yanasema kuwa ‘kipofu hawezi kumuongoza kipofu mwenzake kwa kuwa watatumbukia wote shimoni,’ watoto uwa kama vipofu na uhitaji kupata mtu wa kuwashika ili wasiweze kutumbukia shimoni. Mzazi aliye kipofu ni lazima ataishia kuwatumbukiza watoto wake katika shimo.
Yohana 3:16 inazungumzia juu ya Mungu ambaye ni kiongozi bora na kiongozi makini  na katika uongozi wake anaona ni muhimu kupata kiongozi wa kuongoza familia yake na anamtoa mwanae pekee ili kila anaemwamini na kuwa chini ya uongozi wake hasipotee. Kupotea kwa watoto ni matokeo pia ya kukosa viongozi bora na viongozi wanaoijua njia.
Laweza kuwa fumbo kubwa kulifumbua juu ya kuijua njia ila kuijua njia katika sehemu hii umaanisha kufahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Mungu kwako kwanza kama mzazi na kisha kufahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Mungu kwa watoto wako na pia kuangalia kuyafanya hayo yaliyo mapenzi ya Mungu; na pia kuijua njia ni kufahamu njia ambayo itamsaidia mtoto kukua katika makuzi yaliyo mema na kufahamu nini kama mzazi ufanye ili kuimalisha makuzi mema katika familia yako.
Ni vyema kufahamu kuwa kiongozi/mzazi hana njia moja tu katika kumkuza mtoto bali huweza kutumia njia mbalimbali kuhakikisha mtoto anakuwa katika makuzi yaliyo mema na salama mbele za Mungu. Anaweza tumia njia ya kidemokrasia pale inapobidi na kutumia njia ya kidikteta pale inapobidi, ila kutumia njia moja tu kwa kila jambo ni makosa na ni kukosa kuijua njia kama kiongozi.
Hautoweza kuongoza familia yako kama haujui njia kwa kuwa hasiyeijua njia ni kama kipofu na kipofu hawezi kuongoza kipofu mwenzake. Ila ni vyema kujua kuwa njia njema ni neno la Mungu, kwa kulisoma na kulitafakari kama mzazi na kuliweka ndani linakupa ufahamu wa kuijua njia ili uweze kuwasaidia na wengine kuijua njia.
Zaburi 119:105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, ni mwangaza wa njia zangu.” Ni kwa kulifahamu neno na kuliweka ndani ya moyo ndipo kiongozi anaweza kuwaongoza na washirika wake wakaijua njia sahihi.
Nafasi ya mzazi katika kuijua njia ni nafasi ya kutafuta yeye mwenyewe kujifunza ili aweze kuwafundisha na watoto wake.
Kimtokacho mtu ni kile kilichoujaza moyo wake, ni busara kwa mzazi kujaa neno la Mungu ili kuwasaidia watoto wake na pia hauwezi kutoa kitu ambacho wewe mwenyewe hauna ndani yako, ila waweza kutoa ulichonacho tu, wayapokeayo na kujifunza kwako ni yale uliyonayo.

Kutembea katika njia
Haiishii katika kuijua njia ila inakwenda mbali zaidi katika kutembea katika hiyo njia, yaani kuyafanya yale uyajuayo. Katika kutafuta kuyajua yapi ni sahihi na yapi si sahihi ni vyema kwa kiongozi kuyatenda yale hayajuayo kuwa ni sahihi.

Maxwell anasema kuwa, “wafuasi umwamini kiongozi na kumfuata kuliko vile wanavyojiamini wao wenyewe,”

jambo hili ni vyema sana kwa mzazi kama kiongozi kulifahamu kuwa mara nyingi watoto uwaamini wazazi wao na kupenda kuwaiga hata kama hawako sahihi kwa kuamini kuwa kama yanafanywa na wazazi wao haina shida kwa wao kuyafanya, hata ukiwauliza watajibu mbona hata Baba/Mama anafanya.
Nimeshawahi kuhojiana na watu wengi sana na wengine wakiwa wakubwa kabisa na ukiwaambia kwa nini unafanya kitu Fulani wao utoa jibu kwa kusema, “hata wazazi wangu walifanya hivi hivi.” Kazi ya mzazi ni kuishi katika njia iliyo sahihi ili watoto wake wapate kuona na kujifunza kwa kuiga kutoka kwao.
Wengine wanasema “fuata maneno yangu, usifuatishe matendo yangu,” msemo huu utumiwa na jamii ya watu walioshindwa kufanya yale yaliyo mema na yawatokayo vinywani mwao. Baba mmoja wa kiroho aliyewaongoza watu wengi aitwaye Paulo kwa ujasiri alisema, “nifuateni mimi kama mimi navyomfuata Kristo” kwa maana nyingine yeye kama mzazi alijua na kufahamu kuwa ni jukumu lake kutembea katika njia na akahimiza watoto wake watembee katika njia kama yeye anavyotembea. Na pia mtume Paulo anasema juu ya watu waongozoa kuwa waigwe mwenendo wao ulivyo mwema katika Kristo, na waongozwao waangalie sana mwisho wawaongozao kwa vile wanavyoenenda. Ni vyema sana kwa wazazi kufahamu njia na kutembea katika njia na kuwa makini katika yale wasemayo yaendane na yale wayatendayo.
Wazazi wengi wamekuwa na kasumba ya kuwakemea watoto wao wanapokosea na kuwapa vitisho vikali kwa yale mabaya wanayokuwa wameyafanya, na wengine husema. “ukirudia tena nitakuchapa,” ila watoto wanaporudia maneno hayo ya mzazi hayatekelezwi na mara nyingi wazazi uishia kupiga kelele na kutoa vitisho tena na tena, hali hii ya kushindwa kutembea katika maneno ayasemayo mzazi uwasababisha watoto kuwazoea wazazi na kutoona uzito katika mambo wayasemayo ila jambo la msingi ni kwa mzazi kutimiza kile alichokisema kwa kuwa itamsababisha aaminike katika yale ayasemayo na kumtia hofu mtoto kila anapofanya kosa. Na si katika upande huu tu wa adhabu bali hata upande wa ahadi njema umfanya aamini kuwa wewe ni mtu makini na mtekelezaji wa yale uliyomuahidi.
Wazazi wangu walitulea kwa namna ya kutufanya kuogopa sana kukosea na kuwa makini sana katika mambo tuyafanyayo kwa sababu ya ule ukali waliokuwa nao pale tulipokuwa tunafanya makosa, wakati Fulani mimi na kaka yangu tulifanya kosa na Mama akatuambia kwa kuwa mmefanya hilo kosa leo hamtolala ndani, na alikuwa akimaanisha sana katika adhabu aliyoadhimia na katika kuadhimia huko alifunga mlango na sisi tulikuwa tumekaa muda mrefu nje, tukisubiri labda aweza fungua ila hakufungua mpaka tukaamua kutembea usiku kwenda kulala kwa dada  (binamu) yetu, kwa kupokea adhabu ya namna hiyo ilitufanya tumuone mama kuwa ni mtu anayemaanisha sana na ilitupa kuwa makini sana na kukosea tena. Na alipokuwa akitisha tena tulikuwa makini maana tulijua atafanya.
Mfano wa Mungu kama kioo cha wazazi akiahidi ni lazima atatenda, na akisema ni lazima atafanya na hii ni sababu inayozidi kumfanya Baba yetu kuonekana ni Mungu amaanishaye.
Mtoto akikosea usiache kumpa adhabu ili aogope kurudia tena, hii ndiyo staiki ya mtoto na ndiyo njia bora ya kumkuza mtoto.
Kuonyesha njia
Kazi nyingine kubwa na ya msingi sana kwa mzazi ni kuonyesha njia kama kiongozi kwa kuwa kiongozi bora ni lazima aonyeshe njia kwa wale anaowaongoza, haishii kuijua njia ila uzidi kwa kuionyesha njia kwa wale anaowaongoza. Kuonyesha njia ni kwema na ni tendo ambalo si la siku moja au mwaka mmoja bali uwa ni tendo endelevu kwa nyakati zote ambazo mzazi huwa pamoja na mtoto wake.
Description: a..
Kielelezo no: 1 Mfano wa picha ya mzazi akiwa kiongozi kwa mwanae na mtoto kuvaa kama vile alivyovaa mzazi wake. Baba anaijua njia, anatembea kwenye njia na anaonyesha njia. (Like a father, like a son)
Isaya 48:17 “……..Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.” Mungu kama mzazi mkuu anaonyesha mambo yenye uwiano kwa kufundisha njia ili upate faida na kuionyesha njia ipasayo, hii ni kusema kuwa yeye uhifahamu njia ndiyo maana uionyesha lakini pia anatembea katika njia.
Namna mzazi anavyoweza kuonyesha njia kwa mtoto akiwa kama kiongozi.
Ø  Kwa matendo yako.
Kama mzazi ni muhimu sana kuwa makini sana na matendo unayoyafanya kwa kuwa katika yale unayoyafanya unaweza mjenga au kumbomoa mwanao/wanao. Maandiko yanasema kuwa, “alivyo mchungaji ndivyo walivyo watu wake.” Watoto wao huwa na tabia ya kuiga sana na hupenda na wakati mwingine hujisikia fahari sana kufanya yale ambayo hufanywa na wazazi wao, wengine wakiwa katika michezo na marafiki zao huweza kurudia yote waliyoyaiga kwa wazazi wao, kuwa makini kuijenga tabia ya watoto wako kwa kufanya yaliyo mazuri machoni pao ili waweze kuiga yale yaliyo mazuri kutoka kwako kama kiongozi wao.
Katika matendo kuwa makini sana na aina ya mavazi unayoyavaa kwa kuwa watoto pia hupenda kuiga wazazi wao au watu wakubwa wanavaaje na ni mara chache sana wakaweza kujisimamia katika maamuzi ya wavaaje, haswa kwa wale walio juu kuanzia miaka 12 na kuendelea. Kama mzazi unapenda kuvaa vimini/vinguo vifupi vifupi na vyenye kubana, na vionyeshavyo baadhi ya maungo nje; ni rahisi sana kwa mtoto wako kuiga hiyo tabia na kuanza kuvaa hovyo hovyo na kushindwa kujizuia katika mavazi ayavaayo. Kiongozi anayevaa vibaya ni rahisi kwa wafuasi wake kuvaa vibaya ila kwa kuvaa vizuri usababisha hata wafuasi wake kuvaa vyema.
Hauwezi kubadilisha mtu kama wewe mwenyewe haujabadilika, kama mzazi ni mvaaji vibaya ni vyema akabadilika kwa kuwa yeye ni muonyesha njia kwa kuvaa vibaya uonyesha njia ni kwa namna gani watoto wake wanapaswa kuvaa. Si mavazi tu bali katika maeneo mengi sana ya maisha mzazi ana nafasi kubwa ya kumsaidia au kumharibu mtoto kwa matendo yake, kwa mfano vipindi vya redio, au television uviangaliavyo kama muonyesha njia ndivyo unaweza mjenga au mharibu mtoto wako.
Kama muonyesha njia jitahidi watoto wako wajue misimamo yako kama kiongozi wao na uwawekee mazingira ya kuifuata misimamo yako kwa kuwa wewe ndiye mtoa dira ya ni kwa namna gani wanapaswa kuwa.
David Oyedepo anasema, “wazazi wanapaswa kuwaongoza watoto wao kwa wao wenyewe kuwa mfano kwa matendo yao kwa kuwa watoto uiga sana kile kinachofanywa na wazazi wao.”


Ø  Kwa maneno.
Ulimi ni kiungo kidogo sana ambacho kinauwezo mkubwa wakuharibu na pia kinauwezo wa kujenga, kwa ulimi wako kama mzazi waweza mjenga au kumharibu mtoto wako. Chiriku ni aina ya ndege mwenye uwezo wa kuiga sauti ya mwanadamu kwa jinsi anavyoongea japo hushindwa kutaja maneno katika kuiga huko. Ndivyo alivyo mtoto kwa kuwa ni mtu ambaye hupenda kuiga sana maneno yanayosemwa na wazazi wake, wakubwa na hata wadogo wenzake na ayasikiayo kwenye vyombo vya habari. Ni muhimu kwa mzazi kuwa makini kwa maneno anayosema mbele za mtoto, na pia kumjengea mazingira ya kutosikia maneno machafu yanayoweza kuharibu tabia njema.
Kwa nyakati za sasa imekuwa ni kawaida kuona mtoto anatoa maneno mazito na mengine huwa machafu, na ni kawaida sana kuona mtoto anashinda kijiweni na wakubwa na kutaniana nao na kuwatukana matusi makubwa na wao kumtukana matusi makubwa pia, sababu kubwa ni kuwa, watoto hupenda kuiga na katika kuiga kwao uathiriwa na aina ya yale maneno wanayoyaiga.
1 Wakorinto 15:33 “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya uharibu tabia njema”. Mazungumzo mabaya yanaweza yakawa katika familia au nje ya familia ila huwa na mchango mkubwa sana wa kuharibu tabia njema. Kama kiongozi wa mtoto ni lazima uangalie kumsaidia mtoto kutosikia sikia maneno mabaya ambayo yanaweza haribu tabia yake na hata akawa mtu mbaya.
Wapo wazazi ambao hupenda kuwatamkia watoto wao maneno mabaya na ya kuwakatisha tamaa, kwa mfano, wengine uwaita watoto wao ‘mbwa,’ ‘kenge,’ ‘nyau’, ‘chizi’, ‘mwehu’ na majina mengi mabaya kwa sababu ya kuudhika na makosa ya watoto wao, na wengine uwatamkia ‘sura mbaya’ au kuwakosoa katika baadhi ya maumbile yao kuwa ni wabaya. Wakati wanayasema hayo wao uona ni kawaida sana ila kwa mtoto mambo yale uenda ndani ya mioyo yao na wakati mwingine ujirudia rudia ndani yake na kujiona kuwa hawana hata thamani kabisa kwa kule kufananishwa kwao na vitu visivyo na thamani. Kuna wengine wameamua kuuza utu wao kulingana na kule kutamkiwa kuwa ni wabaya na wenye maumbile mabaya na hawakuona thamani yao ndio maana ikawa ni rahisi kwao kuuza utu wao na miili yao kwa kuwa kwao  kitu cha kawaida na hakina thamani. Kwa maneno ya namna hii wapo ambao ukumbuka hata katika ukubwa wao na kusumbuliwa sana na maneno hayo hata ije neema ya Kristo iwatoe.
Katika jambo kama hili ni muhimu sana kwa wazazi kuwa makini sana na vile wanawatamkia watoto wao kwa kuwatamkia maneno mazuri, mazito na ya kuwatia moyo, ambayo yanawasababisha kujiamini na kuwa watu watofauti hata mbele za wenzao. Watamkie Baraka na mafanikio na maneno mazuri kwa kuwa yatasababisha kujiona wao ni watu wakubwa na watofauti katika ulimwengu huu, wafanye waijue thamani yao na thamani ya miili yao itawafanya waifunike vyema na kuiheshimu ili wengine waiheshimu na kuiogopa. Maneno unayoyatamka yanawatengenezea kesho yao au katika utu uzima wao watakuja kuwa watu wa namna gani, watamkie wao wakisikia na zaidi watamke mbele za Mungu. 
Ni wewe ndiye unayeweza kuwafanya wajijue wao ni wakina nani na wanathamani gani katika ulimwengu huu na miili yao ina thamani gani, kwa kufanya hivi utatengeneza watoto wenye kujiheshimu sana na kujiheshimu kwa watoto ni utukufu na heshima kwa wazazi na Mungu, ila kutojiheshimu kwao ni aibu kubwa kwa wazazi na hata kumuaibisha Mungu aliyewaumba. Kwa mfano mtoto anayevaa vibaya na kuacha maungo yake yapaswayo kufunikwa wazi ni sawa na kuwaweka wazi wazazi wake kwa kuwa hata watu wanaponyooshea kidole utaja kuwa Yule ni mtoto wa Fulani, uzinzi na kila aina ya uchafu aibu yake uenda kwa wazazi wake, mlee mtoto vyema aje kukuletea heshima.
Nimeshawahi kuona wazazi wanaofurahia watoto wao wanapozini, wanapopigana na watu nakuwashinda(ugomvi), na mambo mengine kwa kuamini kuwa kwa kufanya hivyo ni ujanja na kwenda na wakati na wengine wakiona wanavaa vibaya huona kuwa wanaenda na wakati ila si kweli kwa kuwa kwa kufanya hivyo mtoto uingia katika aina ya tabia ambayo si njema, na huweza kumfanya mtu kuharibikiwa na kupoteza muelekeo wa maisha yake.
Ø  Katika uchaguzi wa marafiki
Mtoto katika utoto wake bado hutegemea sana uongozi wa wazazi wake katika uchaguzi wa marafiki kwa kuwaelekeza kuchagua ni marafiki wa aina gani wanapaswa kushirikiana nao na kuwa pamoja nao. Kuna umuhimu wa uhusika wa moja kwa moja wa wazazi kwa kuwa katika hali ya utoto mtoto huweza kuambatana na chochote kile ila kwa muongozo wa wazazi anaweza kujua ni yapi ya kuambatana nayo, na ni yapi ya kuachana nayo.
Tabia ya watoto wote ni kupenda kucheza na katika kucheza huko huweza kukutana na wenzake wenye tabia mbalimbali na wakachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu tabia njema aliyotoka nayo nyumbani. Kama mzazi kuwa makini sana kuona mtoto wako anashirikiana na marafiki wa aina gani akiwa nyumbani, shuleni, kanisani na maeneo mengine mengi.
Usimzuie kucheza kwa kuwa kucheza ni sehemu ya msingi sana kwa mtoto, ila muongoze katika usahihi wa watu wa kucheza naye, mfanye kufahamu anapaswa kucheza na watu wa aina gani.

Marafiki wabaya uharibu tabia njema kwa yale wanayoweza kuzungumza naye, na hata yale afanyayo mengi uchangiwa na marafiki. Angalia sana ni marafiki wa aina gani anaoshirikiana nao na msaidie kukwepa kila aina ya marafiki isiyo na maana, marafiki wabaya ni pamoja na wale walio na ushawishi mbaya juu yake na kuitetea dhambi na kuona ni kitu cha kawaida sana na kutaka ionekane kama ni kitu cha kawaida kwa mwenzake. Hofu ya Mungu ndani yao imepotea na uona mambo ya Mungu kama ni vitu vya kawaida sana na hata akikosea hawawezi kumkosoa ila wanaweza kumtia moyo. Kufahamu zaidi kuhusu mrafiki pata kitabu changu cha ‘huyu ndiye adui wa mafanikio yako’.
2.    RAFIKI
Licha ya kuwa kiongozi na mzazi kwake, mtengenezee nafasi ya kuwa rafiki yako ili uwe rafiki wa karibu kuliko marafiki wote alionao katika maisha yake. Mfano wa kuigwa ni  Mungu, kwa kuwa yeye ni kiongozi, mwalimu, mpaji, Baba (mzazi) ila mara zote uitafuta nafasi ya kuwa rafiki yetu. Ukiwa rafiki kuna mambo atakushirikisha kwa kuwa U rafiki yake, na mambo hayo kamwe hasinge kushirikisha kama ungekuwa mzazi tu, au kiongozi tu, au mkufunzi tu. Watoto wengi wanapoanza kukua na kuingia katika ujana ukutana na mabadiliko makubwa ya miili na viungo na katika mabadiliko hayo uwachanganya sana kwa kuwa huja na uhitaji mkubwa wa kimwili na utafuta sana watu wa kuwashauri na washauri wengine walio wengi uishia kuwashauri vibaya katika kukabiliana na mabadiliko hayo na huwa ni sababu kubwa ya wengine kupotea wanapoingia katika rika hili; utakopofanikiwa kuwa rafiki yake ataweza kukushirikisha na utapata kumsaidia. Ila si wote ambao wanaweza kusema mpaka wachokozwe ila kuzingatia jinsia ni busara kwa kijana wa kiume kuwa na baba na wa kike kuwa na mama.
Description: th

Kielelezo no 2: Mfano wa baba na mtoto katika urafiki, na kutoka pamoja.

Dr. Mayle Munroe anapendekeza miongoni mwa njia njema ya kuwavuta karibu watoto ni kufanya kama marafiki kwa kukaa nao chini na kuzungumza kuhusu maisha. Na kujua vipi wanakwenda na mtazamo wao kuhusu maisha ni upi. Kila siku unayokaa na watoto wako unawatengenezea kumbukumbu, sasa ni kumbukumbu za aina gani ambazo unataka wawe nazo? Unataka watoto wako wakukumbuke vipi katika miaka ijayo; kama mzazi anayeweza kucheka na kuchekeshana na kuwapenda wao kwa uwazi au vinginevyo.”


3.    MKUFUNZI

Licha ya kuwa kiongozi na rafiki mbele za mtoto, mzazi pia ana nafasi kama mkufunzi au mshauri. Katika harakati za kukua mtoto atakuwa anajipatia waalimu wengi sana ila si kujipatia wazazi wengi maana wazazi ni wale wale na hauwezi kuwabadilisha. Wazazi ndio walimu walio wakuu, yaani mwalimu mkuu na msaidizi ni wazazi, na waalimu wengine wao huja kama walimu wakawaida tu. Kwa kuifahamu nafasi hii ni vyema kwa mzazi kuwa makini sana kwa namna anavyoweza kumfundisha mwanae ili awe salama.
Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”. Biblia inasisitiza katika kumlea mtoto katika njia impasayo kwa kuwa hataiacha akikua, inapozungumza juu ya kumlea inagusa maeneo ya kumfundisha, kwa kuwa ulezi ni pamoja na kumfundisha, kumuelekeza, kumuonya, nakadharika.
Description: t
Kielelezo no 3: Mfano wa mzazi kama mwalimu kwa watoto wake.
Ninapozungumzia mwalimu sina maana ya kufanya kama wafanyavyo shuleni, japo hiyo inaweza kuwa sehemu tu, ila maana yake kwa jumla na kwa mapana ni kumuelekeza juu ya yale mema yote anayopaswa kuyafanya na kumpa elimu ili iwe uzima juu yake. Kujifunza uambatana na mazoezi, majaribio kwa kufahamu kuwa yale umfundishayo kama yamemuingia. Yapo maeneo mengi sana ya kujifunza kama, kupika, kufua, kuosha vyombo (kazi za nyumbani), elimu ya kijinsia, na kazi nyingine nyingi za mikono, ila pia kufundisha tabia njema kama kuheshimu wakubwa na kuwasalimia, kutii na kuheshimu mamlaka yoyote iliyo juu yao, kuwa msikivu, kusaidia na kuwapenda wengine na zaidi kumfundisha kweli yote iliyo ndani ya neno la Mungu.
Elimu ya namna hii uchangiwa sana na wazazi kama watu wa karibu ya mtoto, hivyo mzazi ni vyema kujiimarisha na kulitenda eneo hili kwa ufanisi mkubwa. Pia sehemu hii ina uwiano mkubwa sana na ile sehemu ya uongozi kwa njia ya matendo kwa kuwa mwalimu anapaswa pia kuambatanisha matendo yake na yale ayanayo yafundisha ili iwe rahisi kwa watoto kuelewa somo.
Wekeza pia mafundisho ya kutosha uwafundisha kuhusu elimu ya jinsia kwa kuwa wanasikia na kuona mambo mengi kuhusu jinsia zao. Kumbuka wewe ni mwalimu mkuu ni lazima usimame na wewe kumfundisha ni vipi anapaswa kuwa.
Kimtokacho mtu ni kile kilichoujaza moyo wake na hauwezi kumpa mtu kile ambacho hauna ndani yako, kama mwalimu kwa mtoto ni vyema kujaza yale yaliyo mema. Katika eneo la ukufunzi mzazi uweza tumia njia mbalimbali ili kumfanya mtoto ajifunze.

4.    MHUDUMIAJI/MPAJI.
Nafasi nyingine ya mzazi ni nafasi ya mpaji kwa mtoto wake na hii ni nafasi ya Mungu kwa watoto wake kwa kuwa Mungu ni mpaji na mhudumiaji wa watoto wake. Katika nafasi hii ya kuhudumia watoto, mzazi usimama kama mpaji kwa kuhakikisha anawapatia mahitaji yote watoto wake wanayoyahitaji na ni jambo la msingi kwa mzazi kutoa ili mtoto apokee.
Description: f
Kielelezo no 4: mfano wa wazazi katika nafasi ya uhudumiaji, akiwapatia watoto wake fedha.
Zipo huduma nyingi ambazo mzazi anahusika moja kwa moja kumpatia mtoto na huduma hizo zipo katika eneo la chakula, mavazi na makazi. Mbali na hapo mzazi uhusika kuhakikisha anampatia mtoto elimu kwa kumsomesha na mahitaji mengine mengi ambayo uingia katika haya.
Kama mzazi atashindwa kumpatia mtoto wake mahitaji yake ni rahisi kwa mtoto kutafuta wahudumiaji wengine ili wapate kumpatia mahitaji hayo, na wahudumu hao wanaweza kumuathiri vibaya mtoto wako kwa kumpatia mahitaji yake kwa masharti ya kumharibu kitabia na mwenendo.
Wakati Fulani kuna msichana alikuja kwangu na kuanza kulalamika juu ya wazazi wake ambao wameacha kufanya kazi yao ya upaji kwake, na katika kuzungumza nae alionyesha anauhitaji mkubwa hata kuwa radhi kupata mwanaume anayeweza kumsaidia kupata mahitaji yake na alijikuta anaingia kwenye mahusiano kutokana na uhitaji alionao. Ili ni tatizo kubwa sana kwa walio wengi ni vyema kwa wazazi kujitahidi sana kuwahudumia watoto wao vyema huku wakiwafundisha kuridhika na kuwa na kiasi, na katika hili wazazi wazingatie kuwa na idadi ya watoto ambayo wataweza kuhimudu na si kuzidisha ikaja kuwashinda katika kuihudumia.
Wazazi wanapaswa kulizingatia sana swala hili, haswa kwa watoto wa kike ambao uwa na mahitaji mengi ambayo utokana na jinsia yao, usiulize maswali mengi sana kwao haswa kwa wababa ndipo umpatie, kwa kuwa kuna mambo mengine hawawezi kukuambia na kama hautotoa kwa kuwa hawajakuelezea utawafanya kuwatafuta marafiki wakiume ambao watawashirikisha ili wawe wakiwapatia mahitaji yao.
Mungu kama mpaji mkuu aliye mfano wa wazazi anawaambia wanae kuwa, “ombeni nanyi mtapewa………. kwa kuwa kila aombaye hupewa,” hii ni hatua njema kwa mzazi kuifikia japo si kila jambo waweza mpatia aliombalo kwa kuwa akiomba lisilo jema si rahisi kumpatia na pia kuna mengine yapo nje ya uwezo wako kuyatoa ila ni muhimu kufahamu kuwa ukiombwa ni vyema kutoa kwa kuwa ni mpaji kwake ila tu kama yapo ndani ya uwezo wako.
Kiongozi mmoja wa kiroho alishuhudia kwa namna anavyosimama katika nafasi hii ya upaji kwa watoto wake na kusema ni kwa namna gani utoa mahitaji ya watoto wake pale wamuombapo na afanyapo hivyo hujisikia vizuri kwa kutimiza wajibu wake kwa watoto wake na hutiwa nguvu zaidi anaposikia neno ‘ahsante’ kutoka kwa wapokeaji wake na humpa nguvu ili kufanya zaidi na zaidi. Neno ahsante si kwa wazazi wa kimwili tu hata kwa Mungu aliye mbinguni hupenda sana watoto wake wanaposema ahsante pale anapotoa mahitaji kwao.
Katika kutoa huduma mzazi ni lazima kuangalia na kukwepa sana kuwa na upendeleo kwa watoto ila kwa watoto wa kike ni vyema sana kupewa vipaumbele vya utofauti kulingana na mahitaji yao kuwa ni mengi ukilinganisha na walivyo watoto wa kiume, ukaribu na huduma njema kwao ni ulinzi wa kutoharibikiwa.
Kuna hadithi ya zamani ya kaka ‘M’ alimpatia zawadi rafiki yake ‘S’ na alirudia zaidi ya mara moja na wakati mwingine alimpatia zawadi ya aina ile ile tena, ‘S’ alipoipokea akaiangalia na hakusema neno ahsante bali alianza kumlaumu kwa nini amemletea ya aina ile ile, ‘M’ alitulia kimya pasipo kujibu lolote, akawaza kuwa, kwa nini nilimpa yeye ni bora ningempa mtu mwingine angesema ahsante, tangu wakati ule moyo wake uliingia uzito sana kumpatia ‘S’ kitu chochote, ila kuna mwingine alifanyiwa kitu kidogo sana na ‘M’ alishukuru sana mpaka akamwambia Mama yake, kwake ilimpa nguvu kumthamini huyu wa pili kuliko Yule wa kwanza, Mfano huu ni vyema kujifunza kwao kwa kuwa ndivyo Mungu anavyotuchukulia na sisi kwa tabia zetu za kushukuru.  
Ni jambo la busara kwa mzazi kumfundisha mwanae/wanawe kuwa na shukurani kwa chochote wakipokeacho kwa kuwa ni vyema kwa mtoto kuwa na shukurani kwa kila apokeacho kutoka kwa wazazi wake na watu wengineo, kwa kusema ahsante anasababisha wazazi wake wapate nguvu ya kumuhudumia zaidi, kwa chakula wampatiacho, mavazi wampatiayo, elimu wampatiayo, na mahitaji mengi watoayo kwake ni busara na hupendeza sana kwa mtoto kusema ahsante. Neno asante humtia nguvu sana alipokeaye kutenda zaidi na zaidi. Hakuna mzazi anayependa mtoto asiye na shukurani ila wazazi wote hufurahishwa na neno ahsante.
Katika kupokea ni vyema pia kwa mtoto kuwa radhi na tabia ya kuridhika na kupokea kwa shukurani yale ayapokeayo kutoka kwa wazazi wake. Kuifahamu hali ya wazazi ni vyema sana na kutamfanya mtoto kuwa radhi na kile kinachopatikana.
5.    MPANZI
Mzazi ni kama mpanzi na mtoto ni sawa na udongo, neno la Mungu ni mbegu ipandwayo. Inategemea mzazi amebeba mbegu(neno) kwa wingi gani ili aweze kupanda katika udongo alionao. Neno la Mungu usema kuwa “neno la Kristo likae kwa wingi ndani yenu, kolosai 3:16,” Mzazi ni lazima ahakikishe amebeba neno(mbegu) za kutosha ndani yake ili kupanda na ni lazima awe makini kulitunza shamba lake kwa umakini mkubwa ili aje kupata kile alichokipanda.
Kama ilivyo kwa mpanzi uwa makini kupambana na wadudu na wanyama wote watakao kuharibu mazao yake, ndivyo impasavyo mzazi kuwa ili kulinda shamba lake.
Wagalatia   “Msidanganyike; apandacho mtu, ndicho atavuna,” kamunapanda neno ni lazima utavuna matokeo ya lile neno ulilolipanda na ukipanda mambo ya ulimwengu huu kwa mwanao ni lazima yatakurudia hayo uliyoyapanda tena kwa wingi kwa kuwa mbegu moja ya mahindi uzalisha mahindi mengi sana. Naye lazima atazidi zaidi ya kile alichokipokea. 
6.    MFINYANZI
Pia mzazi ni mfinyanzi na mtoto ni udongo, kama mfinyanzi ubeba picha ya mtoto anapaswa kufananaje na ujishughulisha kuhakikisha kuwa mtoto afinywangaye yupo katika hali njema na ya kulidhisha. Mtoto uwa kwa vile umfinyangavyo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni