Jumanne, Septemba 13, 2016

MCHAWI ALIYEIROGA TANZANIA (SEHEMU YA KWANZA)

KUTOJIAMINI SISI WENYEWE

Kuna kituko ambacho kimebeba umaarufu sana kwenye jamii yetu kwa sasa, kinasema;

“maprofesa walikuwa wakisafiri kutoka eneo moja kwenda eneo jingine, wakawa wamepanda ndege ya pamoja kwa ajili ya kuondoka, muda mchache kabla ya ndege ile kupaa akaja mhudumu na kuwaweka sawa kwa ajili ya safari na kuwakaribisha katika ndege ambayo imetengenezwa na mhandisi aliyemaliza chuo kikuu UDSM, wale maprofesa wote walikuwa wanatokea chuo hiko waliposikia tu kuwa ndege inayotaka kupaa imetengenezwa na mwanafunzi waliomfundisha wakaamua kushuka na ndani ya ndege alibaki profesa onyango. Walipomuuliza mbona anabaki hashuki katika ile ndege akawajibu kuwa kama ni mwanafunzi aliyemfundisha yeye hiyo ndege haiwezi kupaa”

Wale maprofesa wengine waliogopa kubaki mule ndani kwa kuwa waliogopa kuwa ile ndege ni lazima itaanguka tu na aliyebaki alikuwa anaamini kuwa haiwezi kupaa kabisa.

Watanzania wengi sana hatujiamini kuwa tunaweza tukafanya mambo sisi wenyewe na yakawa bora zaidi ila tunachokiamini mar azote kuwa vitu ili viwe vizuri ni lazima vifanywe na watu wa ngozi nyeupe. Hata kuwe na mkataba wa kufanya huwa ni ngumu sana kwa waafrika kuaminiana kuwa wanaweza kufanya ila ni rahisi kuamini kuwa shughuli kama hizo ili ziwe bora ni lazima zifanywe na wazungu.

Tunavyuo vingi sana vinavyozalisha wahandisi wa fani mbalimbali ila huwa hatuwaamini na kuwatumia kuwapa kazi badala yake kazi zetu tunaenda kuwapa wakandarasi wa kutoka nchi za nje kama china, marekani na ujerumani. Ukiangalia sana utagundua kuwa hatuwaamini wakandarasi ambao wanazalishwa kila mwaka na vyuo vyetu na hata wao imewapelekea kutojiamini na hata wakisoma wanaishia kuwaza kuwa wakandarasi wa kujenga nyumba na kusimamia mabomba ya maji na hawawazi kabisa kama wanaweza kupewa nafasi ya kusimamia mambo makubwa.

Kama wakandarasi wa kutoka nje ya nchi zetu wanaweza inashindikana vipi kwa wakandarasi wa ndani ya nchi kushindwa. Ni lazima tuanze kuwajengea uwezo wa kujiamini kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa. Kama tutawaamini na kuanza kuwaachia wafanye wataishi kwa kujiamini na kujipa wajibu wa kugundua mambo mengi zaidi sana.

Kwa mfano kwa sasa Tanzania tunatembea katika kauli mbiu inayoamini katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Swali la kujioji ni, hii nchi ya viwanda itajengwa na wakandarasi kutoka nje ya nchi au wa humu ndani ya nchi. Umefika wakati ambao lazima tukiamini tulichonacho na tuanze kukitumia.

Mbali na masuala ya kiuandisi ukienda katika eneo la afya bado utakuta tatizo ni lile lile. Hivi kama India na Marekani wangekuwa wakiumwa wanawaleta watu wao kuja kutibiwa Afrika ni lini wangetengeneza wataalamu wao wenyewe ambao wangekuwa madaktari bingwa ambao leo hii wamekuwa kimbilio. Au madaktari wan chi kama hizo wanavuta pumzi tofauti na madaktari wa huku kwetu, au wanawazidi kitu gani haswa. Ni kweli kuna sehemu lazima tutakuwa tunazidiwa nao haswa katika eneo la ujuzi, ila tunafanya kitu gani ili kuondoa huo mwanya. Ni lazima tujikite kuwekeza katika madaktari wetu na kufanya namna yoyote ile itakayowasaidia kuwa wagunduzi zaidi.

Ukimsoma Daktari maarufu sana Ben Carson aliyetenganisha mapacha walioungana vichwa utagundua kuwa aliwekeza zaidi katika kufanya utafiti ambao leo hii umemfanya kuwa Daktari maarufu zaidi. Bado naamini inawezekana na sisi tukapata wataalamu zaidi ya Ben Carson kama tutawekeza zaidi katika kujiamini sisi wenyewe zaidi ya kuamini kuwa wazungu tu ndio wanauwezo wa kufanya mambo makubwa kama hayo.

Mara nyingi tumekuwa tukishuhudia wakiibuka vijana wanaogundua vitu vya kiteknolojia, kuna mwingine alitengeneza ndege kabisa, kuna wengine walianzisha vituo vya redio kwa kuunga unga mitambo na ikafanya kazi kama vituo vya redio za kawaida. Pamoja na vitu kama hivyo hawa watu wamekuwa wakiishia kutosikika tena na hakuna anayethamini juhudi zetu kwa sababu hata viongozi wetu hatuamini sana kama wanaweza wakafanya vitu vikubwa. Nchi zinazofanya mapinduzi ya viwanda haziwezi kuacha kupuuza kuwa na watu kama hawa na kuwapatia nyenzo muhimu zaidi wanazozihitaji ili wafanye makuu zaidi.

Rafiki yangu Mabula Jilala wakati akiwa anasoma sekondari kama kidato cha tatu alikuwa na mawazo ya kuja kuwa mhandisi na atengeneze Trekta kwa kuwa alichoshwa na mahangaiko ya kilimo cha jembe la mkono. Na alikuwa akijaribu kufanya hivyo na alianza kuchokonoa injini ya Trekta bila kufundishwa na mtu yeyote na akafanikiwa kuwasha Trekta ilo, ila hakukuwa na mtu wa kutazama juhudi zile na hata watu waliokuwa wakimuona walimtazama kama kijana mtundu tu, na sasa haendelei na ujuzi huo tena.


Tunao wataalamu wengi sana katika jamii yetu kama tutakuwa makini kuwatumia itasaidia kweli kuwa nchi ya mapinduzi ya viwanda.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni