Ijumaa, Julai 22, 2016

JIFUNZE KWA WALIOKUTANGULIA ~Kitaso

JIFUNZE KWA WALIOKUTANGULIA
By, Kelvin Kitaso…. 0713804078, 0769190019




“Kikomo cha mwenye hekima katika kujifunza ni siku anayokufa, lakini mpumbavu hukinai kujifunza yungali anaishi”

Katika maisha kujifunza ni kitu muhimu sana na endelevu, kujifunza si ujinga ila ujinga ni kushindwa kujifunza. Wengi hudhania kuwa kujifunza ni kuingia darasani tu, ila kujifunza si kuingia darasani na ni zaidi ya kuingia darasani. Kwa sababu mtu anaweza akawa darasani halafu asifanikiwe kujifunza na mwingine akawa nje ya darasa akajifunza vizuri zaidi.
Wengi hushindwa kufanya mambo ya msingi yanayoweza kuwasaidia kutoka katika maisha yao kwa sababu ni wavivu kujifunza.

Usionee mtu aibu ya kujifunza hata kama unamzidi umri, mali, fedha, elimu ila kama kuna taarifa anazifahamu kuliko wewe jishushe na ukubali kujifunza kutoka kwake.

“Uvivu wa kujifunza ni chanzo cha ujinga”

Kabla hujaanza kufanya jambo unalohitaji kulianza anza kwa kuwauliza waliokutangulia walifanyaje au wanasemaje juu ya jambo kama hilo, na uliza wengi kwa kadiri uwezavyo hiyo itakufanya kupata taarifa nyingi ambazo zitakufanya kuwa bora zaidi yao na kutakufanya kupunguza wingi wa vikwazo ambavyo ilikuwa ukutane navyo.

Jifunze katika vitabu maana humo kuna taarifa nyingi zimekusanywa, kwa kadiri unavyosoma ndivyo unazidi kupata maarifa yatakayo kusaidia kuyaboresha maisha yako.
Kabla hujaingia kwenye ndoa anza kujifunza kuuliza waliopo kwenye ndoa, soma vitabu ambavyo vitakufanya uwe na taarifa na maisha ya ndoa yapoje, kaa chini na wazazi au walezi wako jifunze kwao na uliza maswali mengi kwa kadiri uwezavyo. Kumbuka kujidhania kuwa unajua sana kutakusababisha kuja kushindwa vibaya sana.

Siku moja nikiwa na rafiki yangu tukibadilishana mawazo kuhusu uzoefu wa maisha ya ndoa katika uzuri na changamoto zake, tukaanza kuzungumzia changamoto ya mwanandoa kutoka nje ya ndoa, kisha akaniuliza kama itanitokea mimi nimejiandaa kukabiliana nayo kwa namna gani? Niliposikia swali hilo nikacheka sana na kicheko kilipokatika nikaingiwa na huzuni na kujihurumia kwa kuwa sikuwahi kuwaza changamoto kama hiyo. Si vitu vizuri kuvizungumza ila ukijifunza mapema lolote litakapokukuta halitokusumbua.

“Kujidhania unajua si kujua”

Kabla haujaanza biashara, kampuni au kiwanda tumia muda mwingi kujifunza sasa maana kuna siku utatamani kujifunza hautopata muda wa kufanya hivyo, jifunze kwa wanaomiliki viwanda wanafanyaje, wanaendeshaje maisha yao, na kila kitu kinachohusu uzalishaji, usambazaji, masoko, kodi, n.k.

Kabla hauja anza kilimo au ufugaji jipe muda wa kujifunza vya kutosha yahusuyo kilimo au ufugaji katika uzuri na changamoto zake.
Unapoamua kujifunza kitu usiegeme upande mmoja, tafuta kufahamu uzuri na ubaya wa hiko kitu, na ujiandae kukabiliana na huo ubaya kwa namna ya kuushinda.
Katika kujifunza uliza swali lolote kwa mtu ambaye anajua zaidi yako maana kuuliza si ujinga na usione aibu maana umekusudia kujifunza. Acha kuitii sauti inayosema sijui atanielewaje, wewe angalia kuwa unapaswa kujifunza.

Katika kujifunza usiangalie mtu, angalia kitu unachotakiwa kujifunza kwa huyo mtu.
Unapoingia sehemu usijifanye wewe unajua zaidi ya wote na ukaanza kupiga kelele na kuongea unayofanya hiyo itakupa ufinyu wa kujifunza, ukifika sehemu kaa kimya kwanza uwasikilize wengine wana nini na wanafanya nini ili upate kujifunza. Penda kusikiliza yaw engine zaidi ya unavyopenda watu wasikilize ya kwako.

Usijidhanie kwamba umejitosheleza, kila siku unapoamka jua kuna kitu kipya unapaswa kujifunza, kaa tulia na ujifunze kwa kusoma, kusikiliza audio, kuangalia DVD, au kwa kuzungumza na kusikiliza kwa wengine. Kama usipoiweka akili yako katika mfumo wa kujifunza hata somo jipya likija hautojua kama unapaswa kujifunza.

Waafrika si Wasomaji wa Vitabu

Msemo huu ni msemo wa ujinga na upumbavu. Unaposema si wasomaji wa vitabu maanaake si watafutaji wa maarifa na mtu asiye na maarifa ni mjinga na anayekataa maarifa ni mpumbavu.
Kunatofauti kati ya mjinga na mpumbavu, mjinga ni mtu asiye na maarifa (hajui/hana ufahamu) ila akipata hayo maarifa hatokuwa mjinga tena.

Mpumbavu ni mtu anayekataa maarifa, yaani anajua kabisa haya ni maarifa na yanasaidia ila yeye hataki.Vitabu ni maarifa ambayo hujenga nafsi, na nafsi ndipo kuna mfumo mzima wa maisha ya mwanadamu yaani mfumo wa utajiri na hata umaskini vyote vyaweza kutokea huko kulingana na aina ya taarifa unazoingiza.

Ukitafsiri sasa ule msemo uliozoewa sana utagundua tafsiri yake ni Waafrika ni wapumbavu (watu wasiotaka maarifa). Msemo huu una ukweli kwa sehemu yake kwa kuwa waafrika wengi hawapendi kujifunza na hata wale wanaoitwa wasomi, usomi wao umeishia katika yale wanayofundishwa darasani tu. Siri kubwa ya kufanikiwa ipo katika kuyapata maarifa na maarifa huja kwa kujifunza na kujifunza huja kwa kusoma, kusikiliza na hata kuona.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni