Jumatatu, Oktoba 03, 2016

FANYA BIDHAA YAKO KUWA BORA ZAIDI.

Dunia hii watu wanaofanya vitu kama unavyofanya wewe ni wengi sana na wanazaliwa kila siku, ila kitu pekee kitakachokutofautisha na hao wengi ni ubora tu.
kuna wahubiri wengi sana ila wanaosifika na kupendwa sana ni wachache, kuna waimbaji wengi ila wanaosifika na kupendwa ni wachache sana, kuna waandishi wengi ila wanaosomwa ni wachache kulinganisha na wingi wa waandishi.
Hakuna kitu kipya utakachotuletea utuambie kuwa ni kitu kipya... hakuna jipya chini ya jua. vyote hivyo unavyoviona vilikuwepo tangu zamani, kazi yetu ni kuviboresha tuvifanyapo na kuvifanya kuwa bora zaidi.
Wakati nimemaliza kitabu changu cha kwanza nilichoanza nacho cha "uungu wa mwanadamu" nilimfuata bishop mmoja na kumuelezea maudhui ya kitabu kile kuwa nina kitabu nimeandika vitu kama vipya maana sijasikia mahali popote nilitulia tu katika kutafakari na Mungu akanipa hiyo!! yule bishop akacheka na kuniambia mbona hakuna kitu kipya yaani ni lazima kutakuwa na wengi tu waliofundisha kuhusu hiko kitu. wakati ule nalikuwa mgeni sana na mitandao na nilikuwa sifahamu mambo mengi sana ukilinganisha na sasa japo kwa sasa pia bado mengi tu sijayafahamu. baada ya miezi kadhaa naliitwa kahama kwenda kufanya huduma, nalipokuwa huko nalikuta kitabu cha Bishop Oyedepo, nilipoanza kukisoma nalikutana na yale mambo niliyoyaandika na ufahamu ukanijia zaidi kuwa yale wewe uyaonayo mapya na kujidhania pengine ni wewe tu unayajua kumbe wapo wanaojua hayo hayo hata zaidi ya vile wewe unayajua.
usiridhike na hiko ulichonacho leo, tafuta kila njia ya kuongeza ubora siku hata siku.
Mwimbaji mmoja alinitafuta na kunieleza kuwa anahitaji kutoa albamu yake ya nyimbo saba hivi, nikamwambia naomba nitumie nisikilize kabla ya kwenda studio japo sina utashi wa uimbaji ila kizuri na kibaya nakielewa tu. niliposikiliza zile nyimbo hazikunipendeza kabisa nikamwambia msaada mkubwa wa kwanza naweza kufanya ni kumpatia mwalimu mwenye uzoefu mkubwa amnoe kabla ya studio. nilipomuunganisha nae wakawa hawaelewani na mwimbaji yule alijiamini kuwa anajua na nyimbo zake zilipofikia hazihitaji kufanyiwa hayo marekebisho. Hapo ndipo tuliponyoosha mikono maana kumfundisha mtu anayejua ni kazi sana.
usiweke chuki wala uhasama na watu waliobora, jisogeze karibu nao hata kwa gharama yoyote ili ikusaidie kuwa bora.
Bora uchelewe kufika lakini ukafika salama kuliko kuwahi kufika huku umepata majeraha.
Mambo mazuri hayahitaji haraka/papara
Hiyo albamu unayoipeleka haraka haraka ili tu itoke 2016 ni bora ungejipa muda wa kutosha ili hata ikitoka 2017 iwe bora zaidi ya sasa.
Hiko kitabu unachokipeleka mbio mbio ili tu kitoke sasa ni bora ungevuta muda kuandaa bidhaa iliyobora zaidi.
Si unafahamu kuwa vitu visivyobora huwa vinaboa.
usifanye vitu kwa kisingizio cha kuwa unakimbizana na muda. Acha kushindana na muda, hakuna aliyewahi kukimbizana na muda akaushinda.
Jipe muda, fanya kwa ubora, hakiki kazi zako mara kwa mara ili utakapokuja kufanya chochote kila mtu avutiwe na kile ulichokifanya.

Alhamisi, Septemba 22, 2016

Unahitaji mshauri ‘mentor’ akusaidie kufika kule unapopaswa kufika

Pale unapohitaji kufika kamwe huwezi kufika peke yako ni lazima upate mentor ambaye atakuwa anakusaidia kukuonyesha njia sahihi ya kupitia. Kama hauna mentor wa kukuongoza, kukushauri na kukusaidia utaangaika kila siku kwenye jambo lile lile na bado hautaona mpenyo.
Ukweli ni kuwa hakuna aliyezaliwa na maarifa na kufahamu kila kitu na ndio maana kila siku na kila saa tunahitaji kujifunza ili tuweze kupata maarifa ya kutusaidia. Unahitaji mentor kwa kuwa kuna mambo mengi sana huyajui kabisa ila huyo mentor atakusaidia kuyajua, atakushauri na hata kukukosoa unapokosoa ili uwe kwenye njia sahihi.

Ukisoma kwenye biblia utaona watu wote waliofanikiwa katika huduma, na hata maisha ya kawaida walikuwa ni watu waliokuwa wakijifunza na walikuwa na watu ambao walikuwa wakufunzi wao na kila mara walikuwa wakiketi chini yao na kujifunza kwao.

“chui huwa anazaa chui mwenzake (a tiger will give birth to a tiger)” uknown

Timotheo na Tito walitumia muda mwingi kujifunza kwa Paulo kabla hawajaanza kufanya huduma (kabla hujaanza kufanya hiko kitu tafuta kujifunza kwa mtu ambaye tayari alikifanya au anakifanya), kabla hujaanza kupita hiyo njia unayotaka kuipitia tafuta kujifunza kwa waliowahi kupita hata kama hawakufika watakuwa na jambo tu la kukusaidia na linaweza kukusaidia usikwame kama wao walivyokwama.

Elisha alitumia muda mwingi kujifunza kwa Eliya kabla hajawa Nabii kushika sehemu ya Eliya (mkufunzi wake) na fuatilia utagundua kuwa muujiza wa mwisho wa kufanywa na Eliya ndio ulikuwa muujiza wa kwanza kufanywa na Elisha wa kuyapiga maji na vazi na kugawanyika na kufanya njia ya kupitia.

Joshua alitumia muda wake mwingi kujifunza kwa Musa kama mkufunzi wake na maandiko yanaonyesha kuwa Yoshua alifanya vizuri sana na hata alipokuwa anaukabiri mto Yordan alikuwa suala gumu sana kuugawanya mto huo watu wapite kwa kuwa alishawahi kushuhudia mkufunzi wake akigawanya bahari ya shamu.

Unahitaji kujifunza kwa waliokutangulia, tumia muda wako mwingi kukaa nao kuna mambo mengi sana watakusaidia kuyajua.

Unadhani kwa nini Mungu alimpa fursa Daudi kutoka porini kuchunga kondoo na mbuzi na kumpeleka kuwa mpiga kinubi kwa mfalme? Bila shaka Mungu alikusudia Daudi ajifunze mifumo na taratibu na mambo ya kifalme ili akiwa mfalme isije kuwa taabu.

Kama unataka kuja kuwa mwanasiasa mkubwa tafuta sana wanasiasa ujifunze kwao, soma na fatilia habari zao, mifumo ya maisha yao, jifunze madhaifu na mazuri yao kabla haujafika, hii itakusaidia kipindi unafanikiwa nawe kuwa utakuwa unauzoefu.

Hata Mungu amuinui mtu tu kutoka shambani na kumpeleka Ikulu moja kwa moja, huwa anamuinua na kumpeleka karibu na watu wa mifumo kwanza ili ajifunze kwanza na akishaona amefuzu ndipo anamuingiza kwenye mifumo. Na ndio maana Yusufu aliuzwa kwa Potifa ili ajifunze namna ya kuwa kiongozi katika nafasi za juu. Pale Mungu anapokuweka si bure ni lazima ujifunze kujifunza kabla hajakuinua kukupeleka ngazi nyingine.

Unapokuwa chini na hujui hata hatua ya kufanya ili usonge mbele muombe Mungu akupe mtu sahihi atakayekusaidia kutoka katika hilo eneo.


Mara zote ni lazima ufahamu kuwa unajifunza kwa kuwa kuna ujinga unao na ujinga huo unatoka pale tu unapojifunza.

Jumanne, Septemba 13, 2016

MCHAWI ALIYEIROGA TANZANIA (SEHEMU YA KWANZA)

KUTOJIAMINI SISI WENYEWE

Kuna kituko ambacho kimebeba umaarufu sana kwenye jamii yetu kwa sasa, kinasema;

“maprofesa walikuwa wakisafiri kutoka eneo moja kwenda eneo jingine, wakawa wamepanda ndege ya pamoja kwa ajili ya kuondoka, muda mchache kabla ya ndege ile kupaa akaja mhudumu na kuwaweka sawa kwa ajili ya safari na kuwakaribisha katika ndege ambayo imetengenezwa na mhandisi aliyemaliza chuo kikuu UDSM, wale maprofesa wote walikuwa wanatokea chuo hiko waliposikia tu kuwa ndege inayotaka kupaa imetengenezwa na mwanafunzi waliomfundisha wakaamua kushuka na ndani ya ndege alibaki profesa onyango. Walipomuuliza mbona anabaki hashuki katika ile ndege akawajibu kuwa kama ni mwanafunzi aliyemfundisha yeye hiyo ndege haiwezi kupaa”

Wale maprofesa wengine waliogopa kubaki mule ndani kwa kuwa waliogopa kuwa ile ndege ni lazima itaanguka tu na aliyebaki alikuwa anaamini kuwa haiwezi kupaa kabisa.

Watanzania wengi sana hatujiamini kuwa tunaweza tukafanya mambo sisi wenyewe na yakawa bora zaidi ila tunachokiamini mar azote kuwa vitu ili viwe vizuri ni lazima vifanywe na watu wa ngozi nyeupe. Hata kuwe na mkataba wa kufanya huwa ni ngumu sana kwa waafrika kuaminiana kuwa wanaweza kufanya ila ni rahisi kuamini kuwa shughuli kama hizo ili ziwe bora ni lazima zifanywe na wazungu.

Tunavyuo vingi sana vinavyozalisha wahandisi wa fani mbalimbali ila huwa hatuwaamini na kuwatumia kuwapa kazi badala yake kazi zetu tunaenda kuwapa wakandarasi wa kutoka nchi za nje kama china, marekani na ujerumani. Ukiangalia sana utagundua kuwa hatuwaamini wakandarasi ambao wanazalishwa kila mwaka na vyuo vyetu na hata wao imewapelekea kutojiamini na hata wakisoma wanaishia kuwaza kuwa wakandarasi wa kujenga nyumba na kusimamia mabomba ya maji na hawawazi kabisa kama wanaweza kupewa nafasi ya kusimamia mambo makubwa.

Kama wakandarasi wa kutoka nje ya nchi zetu wanaweza inashindikana vipi kwa wakandarasi wa ndani ya nchi kushindwa. Ni lazima tuanze kuwajengea uwezo wa kujiamini kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa. Kama tutawaamini na kuanza kuwaachia wafanye wataishi kwa kujiamini na kujipa wajibu wa kugundua mambo mengi zaidi sana.

Kwa mfano kwa sasa Tanzania tunatembea katika kauli mbiu inayoamini katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Swali la kujioji ni, hii nchi ya viwanda itajengwa na wakandarasi kutoka nje ya nchi au wa humu ndani ya nchi. Umefika wakati ambao lazima tukiamini tulichonacho na tuanze kukitumia.

Mbali na masuala ya kiuandisi ukienda katika eneo la afya bado utakuta tatizo ni lile lile. Hivi kama India na Marekani wangekuwa wakiumwa wanawaleta watu wao kuja kutibiwa Afrika ni lini wangetengeneza wataalamu wao wenyewe ambao wangekuwa madaktari bingwa ambao leo hii wamekuwa kimbilio. Au madaktari wan chi kama hizo wanavuta pumzi tofauti na madaktari wa huku kwetu, au wanawazidi kitu gani haswa. Ni kweli kuna sehemu lazima tutakuwa tunazidiwa nao haswa katika eneo la ujuzi, ila tunafanya kitu gani ili kuondoa huo mwanya. Ni lazima tujikite kuwekeza katika madaktari wetu na kufanya namna yoyote ile itakayowasaidia kuwa wagunduzi zaidi.

Ukimsoma Daktari maarufu sana Ben Carson aliyetenganisha mapacha walioungana vichwa utagundua kuwa aliwekeza zaidi katika kufanya utafiti ambao leo hii umemfanya kuwa Daktari maarufu zaidi. Bado naamini inawezekana na sisi tukapata wataalamu zaidi ya Ben Carson kama tutawekeza zaidi katika kujiamini sisi wenyewe zaidi ya kuamini kuwa wazungu tu ndio wanauwezo wa kufanya mambo makubwa kama hayo.

Mara nyingi tumekuwa tukishuhudia wakiibuka vijana wanaogundua vitu vya kiteknolojia, kuna mwingine alitengeneza ndege kabisa, kuna wengine walianzisha vituo vya redio kwa kuunga unga mitambo na ikafanya kazi kama vituo vya redio za kawaida. Pamoja na vitu kama hivyo hawa watu wamekuwa wakiishia kutosikika tena na hakuna anayethamini juhudi zetu kwa sababu hata viongozi wetu hatuamini sana kama wanaweza wakafanya vitu vikubwa. Nchi zinazofanya mapinduzi ya viwanda haziwezi kuacha kupuuza kuwa na watu kama hawa na kuwapatia nyenzo muhimu zaidi wanazozihitaji ili wafanye makuu zaidi.

Rafiki yangu Mabula Jilala wakati akiwa anasoma sekondari kama kidato cha tatu alikuwa na mawazo ya kuja kuwa mhandisi na atengeneze Trekta kwa kuwa alichoshwa na mahangaiko ya kilimo cha jembe la mkono. Na alikuwa akijaribu kufanya hivyo na alianza kuchokonoa injini ya Trekta bila kufundishwa na mtu yeyote na akafanikiwa kuwasha Trekta ilo, ila hakukuwa na mtu wa kutazama juhudi zile na hata watu waliokuwa wakimuona walimtazama kama kijana mtundu tu, na sasa haendelei na ujuzi huo tena.


Tunao wataalamu wengi sana katika jamii yetu kama tutakuwa makini kuwatumia itasaidia kweli kuwa nchi ya mapinduzi ya viwanda.
         UNYOPASWA KUYAFAHAMU KUHUSIANA NA SADAKA YA LIMBUKO

Hii ni sadaka ambayo ni ya mwanzo wa kila pato ulipatalo katika yale uyafanyayo. Kama ni biashara basi yale mapato ya kwanza ni malimbuko yako kwa BWANA, kama ni kazi huwa mshahara wa kwanza, kama ni mazao huwa yale ya kwanza na vivyo hivyo kwa wanyama. Sadaka hii pia kwa nyakati za leo huwasilishwa kanisani.

Ezekiel 44:30 “Na kitu cha kwanza cha malimbuko yote ya vitu vyote, na kila toleo la kila kitu cha matoleo yenu, litakuwa la makuhani. Tena mtampa kuhani sehemu ya kwanza ya unga mbichi, ili kukalisha Baraka juu ya nyumba yako.

Mithali 3:9:10 “Mheshimu BWANA kwa mali yako. Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. 10 Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika kwa divai mpya.”

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kutoa malimbuko, na ukweli ni kuwa hii sadaka ni sadaka ambayo haina kipaumbele kwa watu. Wengi hawafahamu kabisa kuhusu hii sadaka na hata wanaofahamu ni wachache sana wanaoishiriki ipasavyo.

Ukisoma maandiko hapo juu utaona kuna Baraka nyingi sana zinatajwa kuambatana na mtu anayetoa malimbuko. Kwenye kitabu cha Ezekiel anasema Baraka zitakaa juu ya nyumba ya huyo mtu. Kuna tofauti kubwa ya Baraka kukaa na kuja, zinaweza kuja na kuondoka lakini zikikaa hudumu mahali hapo hapo bila kuondoka. Maanaake nyuma ya mtu anayetoa malimbuko si nyumba ya kawaida, ni nyumba iliyojaa Baraka na kila kilichomo ndani yake kimebarikiwa na kila kizaliwacho ndani ya hiyo nyumba kimebarikiwa pia, na hata mgeni akiingia kwenye hiyo nyumba ni lazima abarikiwe. Malimbuko yanavuta Baraka za Mungu kuishi na mtu.

Mtu ambaye kazi yake anaitolea malimbuko hakuna adui anayeweza kuigusa na kufanya chochote kile anachohitaji kukifanya. Mtu wa namna hii kuna kuinuliwa ‘promotion’ nyingi zitakuwa zinafanyika kwa ajili yake.

“kama mazao/mapato yako ya kwanza yamebarikiwa basi lazima vyote vinavyokuja baada ya hayo view vimebarikiwa”

Watu wengi huwa hawaelewi kuwa sadaka huwa zinadai Baraka mbele ya madhabau ya Mungu na ndio maana anayetoa sadaka kwa uaminifu mbele za Mungu maisha yake mara zote siyo maisha ya kawaida.

Dr. Michael Hutton-Wood anaelezea uzoefu wake katika malimbuko kuwa tangu Mungu amemfunulia siri ya kuelewa nguvu ya malimbuko akaamua kuinuka na kutembea katika kanuni ya kutii na kutoa. Yeye kila anapoanza mwaka, mapato yote ya mwezi January lazima ayatoe mbele za Mungu, na ikiwa mapato yake ya kwanza yamekuwa matakatifu mbele za Mungu basi mapato yote yatakayokuja baada ya hapo yatakuwa yamebarikiwa.

Napenda kubarikiwa, kumiliki vitu vizuri kwangu haitoshi, nataka kumiliki vitu vizuri huku nikiwa ndani ya mfumo wa Baraka za Mungu. Namshukuru Mungu kwa kuifunua siri hii katika maisha yangu.

Ukweli ni kuwa mwezi Januari haswa kwenye jamii zetu za Kiswahili huwa maarufu kama mwezi mgumu kifedha kwa kuwa watu wanakuwa wametoka katika msimu wa sikukuu za Christmas na mwaka mpya lakini pia huwa na majukumu ya kupeleka watoto shule haswa kwa wale wenye familia, inakuwa ngumu kumwelezea mtu asiyejua maana ya sadaka kuwa anapaswa kutoa pato lake ili kutakasa mapato yake ya mwaka mzima. Ila sijawahi kumuona mwenye haki ameachwa kwa sababu ya haki yake.

Hata kama umeangaika kupata kazi muda mrefu na imetokea umepata halafu unamadeni mengi usikulupuke kuanza kula hela ya Mungu. Tulia na uipeleke mbele za Mungu (soma tena Ezekiel 44:30), unapoipeleka mbele za Mungu unasababisha Mungu awe anaiangalia kazi yako kwa umakini, atailinda kazi yako, hata kama kuna watu wanataka kuipoteza haki yako ya kufanyiwa promotion hawatakuwa wanapambana nawe bali watakuwa wanapambana na Mungu mwenyewe na utapewa hata hekima ya kutumia mshahara wako ili isiwe kama wale walioweka fedha zao katika mifuko iliyotoboka toboka.

Hagai 1:6 “Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hakuna aonaye moto; na yeye apateye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka.”

Bila shaka umeshawahi kukutana na mtu anakwambia toka aanze kufanya kazi haoni faida yake, hata mshahara anaoupata haujawahi kufanya kitu chochote cha maana. Siri imejificha humu katika utoaji. Maana Mungu anasema atamkemea yeye alaye ila kama tukitoa zaka na dhabihu, sasa atakemewaje yeye alaye kama mtu hatoi?


Mungu anaheshimu sana pale unapoamua umuheshimu kwa kile ulichonacho na ndio maana kwenye Mithali 3:9-10 anasema akiheshimiwa kwa malimbuko yetu ni lazima ghala zetu zijazwe kwa wingi na kufikia viwango vya kufurika.